In Summary

Dk Shein alizungumzia masuala mbalimbali ya ikiwamo hali ya uchumi, afya, maji na amani.

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema kuanzia Julai, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) itaanza kutoa elimu ya msingi na sekondari bure kwa wanafunzi wote.

Dk Shein alisema hayo jana katika hotuba yake wakati wa kilele cha maadhimisho ya sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo ilieleza kwa undani jinsi Serikali yake ilivyopiga hatua za maendeleo kupitia faida za Mapinduzi ya mwaka 1964.

Katika hotuba hiyo, Dk Shein alisema kutokana na faida iliyopatikana kupitia Mapinduzi hayo, ameona ni vyema kurudisha heshma ya Mapinduzi kwa kuweka elimu ya sekondari bila ya malipo kama ilivyo kwa elimu ya msingi.

“Kuanzia mwezi Julai mwaka huu hakuna mzazi hata mmoja atakayelipa malipo shuleni, mzigo wote utabebwa na Serikali, tunafanya hivi kwa lengo la kurudisha elimu bila malipo kama ilivyokuwa baada ya Mapinduzi ya Zanzibar,” alisema.

Mbali ya elimu, Dk Shein alizungumzia masuala mbalimbali ya ikiwamo hali ya uchumi, afya, maji na amani.

Uchumi

Akizungumzia hali ya uchumi, Dk Shein alisema katika kipindi cha mwaka 2017, ukusanyaji wa mapato uliongezeka kutoka Sh487 bilioni kwa mwaka 2016 hadi kufikia Sh548 bilioni mwaka 2017 ikiwa ni ongezeko la Sh61 bilioni.

“Katika jitihada tulizoanza kuzichukua mwaka 2011/2012, hivi sasa, utegemezi wa bajeti yetu kwa mwaka 2017/2018, umefikia asilimia 7.3, ikilinganishwa na asilimia 30.2 katika mwaka 2010/2011. Mafanikio haya tuliyopata ni makubwa na ya kupigiwa mfano,” alisema.

Pia alisema kasi ya ukuaji wa uchumi kwa bei halisi, imekua kwa asilimia 7.0 kwa mwaka 2017, ikilinganishwa na asilimia 6.8 kwa mwaka 2016 na pato la mtu binafsi nalo limeongezeka na kufikia Sh1,806,000 ikilinganishwa na Sh1,632,000 kwa mwaka 2015.

Afya

Kuhusu afya, Dk Shein alisema Serikali imefanya juhudi kuhakikisha sekta hiyo inakwenda sambamba na Mapinduzi ya 1964 ikiwamo kuongezeka kwa idadi ya hospitali kutoka tano hadi 12, huku vituo vya afya vikitoka 36 hadi 158.

Alisema miongoni mwa hospitali hizo, zimo za vikosi vya ulinzi na usalama ambazo zinatoa huduma kwa jamii bila ya ubaguzi kwa kila mwananchi.

Maji

Dk Shein alisema bado kuna tatizo la maji licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana nalo.

Alisema kwa mujibu wa tathmini ya matumizi ya maji kwa siku, Unguja na Pemba zinahitajika lita milioni 234.45 lakini uzalishaji uliopo hivi sasa kwa siku ni lita milioni 102.8 kiwango ambacho ni kidogo ikilinganishwa na matumizi halisi.

Alisema kiwango hicho hakiridhishi hata kidogo hasa kwa maeneo ya Unguja ambako kunaonekana kuwa na upungufu makubwa ikilinganishwa na Pemba.

Alisema kutokana na upungufu huo, Serikali imefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wananchi wake wanaondokana na tatizo hilo ikiwamo kutafuta mikopo pamoja na hisani ili ifikapo 2019 upatikanaji wa maji uwe wa kutosha.

Amani na utilivu

Dk Shein alisema kwa kushirikiana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli wataendelea kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inamiarika.

Alisema suala la usalama ni miongoni mwa vipaumbele vikuu vya Serikali zote mbili wakati wote, huku akisisitiza kuwa watatumia nyadhifa zao vyema kuhakikisha wanadumisha amani na Muungano uliopo baina ya nchi mbili hizi.

Awaachia huru wafungwa

Katika maadhimisho hayo, Dk Shein aliwaachia huru wafungwa 12 waliomo katika magereza ya Pemba na Unguja.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Abdulhamid Yahya Mzee inaeleza kuwa, “Kwa uwezo aliopewa chini ya Kifungu cha 59 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Rais ameamuru kuwa kifungo kilichobaki cha walionufaika na msamaha huo, ambao bado wanaendelea kutumikia katika Vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba kuwa kipindi hicho chote kinafutwa na kwamba waachiwe huru.”

Walionufaika na msamaha huo kwa Unguja ni Abdul-Azizi Abdalla Mohamed, Omar Abdalla Nuhu, Ali Khamis Mrau, Mussa Ali Vuai, Hassan Seif Khamis, Nassor Abeid Issa, Jihadi Jalala Jihadi na Edward Jeremia Magaja.

Wengine ni Sleiman Abdalla Amir, Mtumwa Khamis Kaimu, Said Seif Omar na Masoud Seif Nassor.