In Summary

Wagombea wake washinda kwa zaidi ya asilimia 90

Songea/Arusha. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepata ushindi katika uchaguzi mdogo wa marudio wa ubunge katika majimbo ya  Songea Mjini, Singida Kaskazini na Longido.

Akitangaza matokeo hayo Singida Kaskazini, msimamizi wa uchaguzi, Rashid Mandoa amemtangaza Justine Monko wa kuwa mshindi baada ya kupata kura 20,857 sawa na asilimia 93.5.

Amesema wagombea wengine na kura walizopata katika mabano ni Dalphine Mlewa wa CUF (974),  Aloyce Nduguta wa Ada-Tadea  (265), Omar Sombi wa AFP (116) na Mchungaji Yohana Labisu wa CCK kura 86.

Amesema kura zilizopigwa ni 22,298, waliojiandikisha kupigakura ni  91,518, “watu 69,220 ambao ni zaidi ya asilimia 70 hawakujitokeza kupiga kura.”

Katika jimbo la Songea Mjini, msimamizi wa uchaguzi, Tina Sekambo amemtangaza Dk Damas Ndumbaro kuwa mshindi kwa kupata kura 45,762 sawa na asilimia  97.

Amesema  Christina Thinangwa wa CUF amepata kura 608 huku Neema Tawete wa ADA-TADEA akipata kura  471 na kubainisha kuwa waliojiandikisha kupiga kura walikuwa

128,841.

Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Longido, Jumaa Mhina amemtangaza Dk Stephen Kiruswa kuwa mshindi baada ya kupata kura 41,258 sawa na asilimia 99.1.