In Summary

Katibu wa Bunge Stephen Kigaigai amesema kuwa bado hawajamuandikia barua ya kumwita kufika katika kamati hiyo.

Dodoma. Bunge bado halijamuandikia barua ya kumuita Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka ili kujibu tuhuma za kukejeli na kudharau muhimili huo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi, Katibu wa Bunge Stephen Kigaigai amesema kuwa bado hawajamuandikia barua ya kumwita kufika katika kamati hiyo.

"Niko katika kikao lakini ninachofahamu kuwa bado hatujamuandikia," amesema Kigaigai.

Januari 9 mwaka huu Spika wa Bunge, Job Ndugai aliagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumuita na kumhoji Sendeka wakati wa uchunguzi wa kamati hiyo kuhusu tuhuma hizo zilizonukuliwa katika mitandao ya jamii kwa lugha ya Kimasai, Kiswahili na Kingereza.

Spika alisema lengo la kumuita ni kubaini ukweli wa dhamira ua kauli hizo na lutoa mapendekezo kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Bunge.