In Summary
  • TRA iliyokuwa ikiendesha mnada huo chini ya kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, imepiga mnada magari hayo baada ya wamiliki wake kutolipia kodi husika ndani ya muda unaotakiwa kisheria.

Awamu ya pili ya mnada wa magari katika Bandari ya Dar es Salaam ilifungwa jana huku baadhi yakikosa wanunuzi kutokana na kikwazo cha bei elekezi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

TRA iliyokuwa ikiendesha mnada huo chini ya kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, imepiga mnada magari hayo baada ya wamiliki wake kutolipia kodi husika ndani ya muda unaotakiwa kisheria.

Mnada huo ulihusisha magari katika vituo vya Malindi, GC Yard, Copper Yard na Mivinjeni vilivyopo ndani ya bandari hiyo.

“Idadi ya magari yaliyouzwa hadi sasa hatujakusanya taarifa zake vizuri, inabidi kukaa na kuangalia, baadaye tutawajulisha idadi, aina ya magari na taarifa nyingine,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Yono, Scholastica Kevela wakati wa mnada huo.

Scholastica alisema kati ya Januari 4 hadi 6, kampuni hiyo iliuza magari 70 kati ya 134 katika bandari hiyo ikiwa ni awamu ya kwanza tangu walipoanza mwaka huu.

Katika mnada wa jana, mwandishi wetu alishuhudia washiriki wa wakishindwa kufikia bei elekezi kwa magari mengi.

Awali, wakati mnada ukiendelea, Scholastica aliruhusu kupandia bei lakini baadaye aliweka wazi kwamba viwango vyao havikuwa zinafikia bei elekezi ya TRA.

Mmoja wa waathirika wa msimamo huo alikuwa Charles Nyanda maarufu Msukuma ambaye awali, alishinda ununuzi wa lori lakini apokonywa.

Msukuma alishinda ununuzi wa gari aina ya Mantrack na tela lake kwa Sh68.7 milioni lakini hakuruhusiwa kuendelea na mchakato wa malipo baada kuonekana kuna makosa yaliyotokana na taarifa sahihi za mnada wa gari hilo, ambalo halikutakiwa kuuzwa kwa bei hiyo iliyoelezwa kuwa ni ya hasara.

“Aliyekuwa mshindi wa gari hili (Mantrack) tuna-nullifiy (tunafuta) gari hilo lilitakiwa kuuzwa kwa bei ya juu zaidi ya hapo, sababu ina tela lake kwa hivyo mnada utarudiwa kwenye utakaotangazwa,” alisema Scholastica huku kukisikika minong’ono ya kutokubaliana.

Hatua hiyo ya kuwekewa bei elekezi iliwakera baadhi ya washiriki hasa wale waliokosa magari kwenye mnada huo, baadhi wakisema Serikali ndiyo itakayopata hasara.

Joseph Kalonga aliyeshiriki mnada huo alisema umekuwa na dosari katika bei ikilinganishwa na ubora wa magari yenyewe na kwamba kwa bei za magari hayo, ni afadhali ya mteja kununua nje.

“Kuna mtu ametaja Sh6 milioni hapa kwa gari aina ya Fan Cargo lakini amenyimwa, wakati gari imekaa hapa hadi imeanza kuoza, tulitegemea mnada wa gari la Sh6 milioni tupate hata kwa Sh5 milioni lakini hakuna,” alisema Kalonga ambaye ni mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam.

Salumu Msambusi aliyeshiriki mnada huo alisema lengo la Serikali ni kukusanya mapato yake hivyo hakuna mantiki ya kulazimisha bei za juu na kusababisha magari kukosa wateja.

“Badala ya Serikali kukusanya kodi inapoteza, wanakataa kuuza gari la thamani ya Sh10milioni leo lakini litakaa thamani yake itaendelea kushuka... kwa hiyo inahitaji umakini sana TRA,” alisema Msambusi.

Hata hivyo, Scholastica aliwataka washiriki ambao hawakupata magari katika mnada huo kushiriki mwingine utakaotangazwa baadaye.