Dodoma. Serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh32.5 trilioni katika mwaka wa fedha 2018/19 ikiwa ni ongezeko la Sh800 bilioni ikilinganishwa na bajeti ya mwaka huu wa fedha ya Sh31.7 trilioni.

Kwenye makadirio hayo, msukumo mkubwa umeelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa reli ya kati iliyotengewa Sh1.4 trilioni.

Akiwasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19 jana mjini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema umezingatia upatikanaji wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali.

Alisema katika mwaka 2018/19, Serikali imepanga kutumia Sh20.4 trilioni kwa matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63 na kwamba kiasi hicho kinajumuisha Sh10 trilioni zitakazotumika kulipa deni la Taifa wakati Sh7.3 trilioni zikiwa ni mishahara ya watumishi na Sh3 trilioni yakiwa matumizi mengineyo.

Alisema Sh12 trilioni sawa na asilimia 37 zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo. Katika fedha hizo, Sh9.8 trilioni sawa na asilimia 82.3 zitatokana na vyanzo vya ndani na Sh2.1 trilioni sawa na asilimia 17.7 kutoka vyanzo vya nje.

Kufanikisha bajeti

Alisema ili kufanikisha bajeti hiyo, Serikali inatarajia kukusanya Sh20.8 trilioni sawa na asilimia 64 kutoka vyanzo vya ndani vinavyojumuisha makusanyo ya halmashauri.

“Kutoka vyanzo vya kodi, Serikali inatarajia kukusanya Sh18 trilioni ambazo ni sawa na asilimia 13.6 ya Pato la Taifa,” alisema.

Kuhusu mapato yasiyo ya kodi, alisema yanatarajiwa kufika Sh2.1 trilioni wakati halmashauri zikitazamiwa kukusanya Sh735.6 bilioni.

Alisema vyanzo vingine vya mapato ni misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo kiasi cha Sh2.6 trilioni sawa na asilimia nane ya bajeti.

Kukopa

Katika mwaka huo wa fedha, Serikali inatarajia kukopa Sh5.7 trilioni kutoka katika soko la ndani. Kati ya fedha hizo, Sh4.6 trilioni zitatumika kulipa hati fungani na dhamana za Serikali zinazoiva.

Alisema Sh1.1 trilioni zinazozidi ndio mikopo mipya ambayo ni sawa na asilimia 0.9 ya Pato la Taifa.

“Kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi, Serikali inatarajia kukopa Sh3.1 trilioni kutoka soko la nje,” alisema.

Miradi itakayotekelezwa

Waziri Mpango aliitaja miradi ya kielelezo itakayotekelezwa kwamba Sh1.4 trilioni zitatumika kuimarisha reli ya kati zote zikiwa ni fedha za ndani.

Licha ya reli, alisema Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limetengewa Sh495.6 bilioni kukamilisha malipo ya ununuzi wa ndege ya pili aina Boeing 787 Dreamliner na Bombardier Q400-8.

Alisema Sh700 bilioni zimetengwa kwa ajili ya mradi wa kufua umeme wa maji katika Bonde la Mto Rufiji, zitakazotumika kwa ajili ya ujenzi wa ofisi, bwawa na njia za kupitisha maji.

Aliutaja mradi mwingine kuwa ni wa makaa ya mawe Mchuchuma uliotengewa Sh5 bilioni ili kufanikisha uzalishaji wa 220KV za umeme na Sh5 bilioni nyingine zikitengwa kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa kiwanda cha chuma Liganga.

Dk Mpango alisema Sh25 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kulihuisha Shirika la Nyumbu ili likarabati miundombinu msingi ya teknolojia na ununuzi wa mashine na mitambo mipya.

Alisema kiwanda cha General Tyre Arusha kimetengewa Sh500 milioni kuandaa upembuzi yakinifu, ununuzi wa mitambo na mashine na kulitangaza eneo hilo kwa ajili ya kupata wawekezaji na kulipa tozo ya ardhi.

Pia alisema mradi wa magadi soda katika Bonde la Engaruka umetengewa Sh10 bilioni kuratibu na kulipa fidia wananchi watakaopisha eneo, kufanya utafiti wa faida za kiuchumi, kusimamia ujenzi wa miundombinu wezeshi, kulipa tozo za ardhi na kulitangaza eneo hilo ili kupata wawekezaji.

Alisema Sh10 bilioni nyingine zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na bidhaa za ngozi huko Zuzu, Dodoma na Sh2 bilioni zitatumika kuliimarisha Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Mpango alisema Kituo cha Zana za Kilimo na Ufundi Vijijini (Camartec) kimetengewa Sh3 bilioni kuendeleza utafiti wa zana za kilimo, kukuza wazalishaji wa ndani wa zana hizo, kujenga miundombinu ya utafiti na kuhakiki ubora.

Ili kuimarisha kilimo, alisema Sh10 bilioni zitatumika kufanya utafiti wa ubora wa mbegu na Sh500 milioni zinatarajiwa kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bandari ya uvuvi.

Changamoto

Pamoja na mipango hiyo, Serikali imetaja changomoto saba zilizoathiri utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa na bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18 ikiwamo malimbikizo ya madai ya watumishi.

Changamoto nyingine ni ugumu wa upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji na matayarisho hafifu ya miradi, mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha uharibifu wa miundombinu ya usafiri kutokana na mvua kubwa zilizonyesha baadhi ya maeneo.

Dk Mpango alisema mwamko mdogo wa kulipa kodi na hususan kuzingatia matumizi ya mashine za kieletroniki kulichangia kutofikiwa kwa malengo ya ukusanyaji wa mapato.

“Masharti magumu kwenye mikopo ya kibiashara kutoka nje na mabadiliko ya sera za misaada katika nchi zilizokuwa zikitupatia misaada ya kibajeti ni changamoto nyingine,” alisema.

Alisema mwaka 2017/18, Serikali ilipanga kukusanya na kutumia Sh31.7 trilioni lakini hadi Januari ilikuwa imekusanya Sh17.4 trilioni sawa na asilimia 85 ya lengo.

Alisema fedha zote zilizokusanywa zilitumika katika maeneo tofauti yaliyopewa kipaumbele ikiwamo kulipa Deni Taifa na mishahara ya watumishi wa umma, kugharamia ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege, kulipa malimbikizo ya wazabuni, makandarasi na watumishi wa umma.

Deni la Taifa

Kuhusu Deni la Taifa, Dk Mpango alisema hadi Desemba mwaka jana, deni hilo lilikuwa zaidi ya Sh47.7 trilioni linalojumuisha Sh34.148 trilioni sawa na asilimia 71.5 ambazo ni deni la nje na Sh13.607 trilioni sawa na asilimia 28.5 za deni la ndani.

Hata hivyo, alisema uwiano wa deni hilo na Pato la Taifa kwa mwaka wa fedha 2017/18 ni asilimia 34.4 ikilinganishwa na ukomo ambao ni asilimia 56.

“Uwiano wa deni la nje na mauzo ya nje ni asilimia 81.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150. Hii inamaanisha kuwa uwezo wetu wa kulipa deni bado ni imara,” alisema.

Alisema Serikali inaendelea kuchukua tahadhari kwa kukopa kwenye vyanzo vyenye masharti nafuu kuhakikisha mikopo hiyo inaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Ripoti ya mapitio ya uchumi ya Agosti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kuwa kwa miezi 13, mpaka Julai mwaka jana, Deni la Taifa liliongezeka kwa asilimia 15 na kufika Sh53.3 trilioni kutoka Sh46 trilioni kwa mwaka ulioishia Juni, 2016.

Kiwango hicho kiliongezeka kutoka Sh52 trilioni za Juni, 2017. Mwaka ulioishia Juni, 2016 deni hilo liliongezeka kwa asilimia 20 kutoka Sh38.2 trilioni zilizorekodiwa Juni, 2015.

Taarifa ya Waziri Mpango, ikilinganishwa na kumbukumbu hizo za BoT, Serikali imetumia zaidi ya Sh5.6 trilioni kulipa deni la Taifa.

Mfumuko wa bei

Akizungumzia mfumuko wa bei, Dk Mpango alisema kulikuwa na utulivu mwaka 2017 kutokana na kuimarika kwa upatikanaji wa chakula nchini.

Licha ya chakula, alisema kulikuwa na utulivu wa bei za nishati hasa mafuta katika soko la ndani na nje ya nchi.

Hadi mwishoni mwa mwaka jana, alisema mfumuko wa bei ulikuwa wastani wa asilimia 5.3 ambao ulipungua na kufika asilimia 4.1 Februari.

Fedha za kigeni

Mpaka Desemba 2017, Waziri Mpango alisema akiba ya fedha za kigeni ilikuwa Dola 5.9 bilioni za Marekani ikilinganishwa na Dola 4.3 bilioni katika kipindi kama hicho mwaka 2016.

“Kiasi kilichofikiwa Desemba 2017 kilikuwa kinatosha kugharamia ununuzi wa bidhaa na huduma kwa miezi sita hivyo kuzidi kiwango cha angalau miezi 4.5 kilichowekwa kukidhi matakwa ya hatua za mtangamano wa umoja wa fedha kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Dk Mpango.

Aidha, mwaka ulioishia Desemba 2017, thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani ilikuwa ya kuridhisha.

Riba za amana

Kwa mwaka ulioishia Desemba 2017, Dk Mpango alisema wastani wa riba za amana ulikuwa asilimia 9.6 ukiongezeka kutoka asilimia 8.8 Desemba 2016.

Hata hivyo, alisema riba za mkopo wa hadi mwaka mmoja, iliongezeka mpaka asilimia 18.2 Desemba 2017 kutoka asilimia 12.9 Desemba 2016. Katika kipindi hicho, alisema riba za amana za mwaka mmoja ilipungua kutoka asilimia 11 Desemba 2016 hadi asilimia 10.9 Desemba 2017.

Baada ya uwasilishwaji huo mawaziri wataanza kuwasilisha mapendekezo ya bajeti zao katika kamati za Bunge za kisekta ambako wabunge watazijadili na kutoa maoni yao.