Tanga. Ziara ya Rais John Magufuli katika Mkoa wa Tanga imekiletea neema kiwanda cha maziwa cha TangaFresh baada ya agizo lake la kutaka kiwanda hicho kitatuliwe changamoto iliyokuwa ikikikabili kwa muda mrefu.

Tangafresh kilikuwa kikikabiliwa na tatizo la kushindwa kukopeshwa kwenye vyombo vya fedha kutokana na hati ya umiliki wa kiwanda hicho kuzuiwa na kamishna wa ardhi kwa kuwa kampuni iliyokuwa ikikimiliki zamani kudaiwa  kodi ya mtaji ya Sh1.2 bilioni.

Rais Magufuli alipokitembelea Jumapili iliyopita  alilalamikiwa na Meneja wa Kiwanda hicho, Michael Karata kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni kuzuiwa kwa hati ya umiliki (Certificate Of Ocupation) na hivyo kushindwa kukopa kwenye benki mbalimbali.

Rais Magufuli hapohapo aliiagiza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhakikisha Tangafresh inakabidhiwa hati hiyo ndani ya wiki moja na kuwakemea watendaji serikalini ambao wanakubali kutumika kuvihujumu viwanda vya ndani ili Tanzania iendelee kuwa soko la bidhaa za nje.

Siku mbili baadaye, kiwanda hicho kilipewa hati hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Alhamisi, Agosti 10 wakati akionyesha hati

hiyo, Meneja huyo alisema aliipokea jana kutoka kwa kamishna msaidizi wa ardhi kanda ya kaskazini.

“Tunamshukuru Rais Magufuli, amri yake imesaidia tumepata hati hii kwa siku mbili tu wakati tuliifukuzia kwa kipindi cha miaka mitano  bila mafanikio,” alisema Karata.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela  alisema ufuatiliaji  wa hati hiyo ulianza baada ya Rais Magufuli kutoa amri.

Tangafresh kinamilikiwa na Ushirika wa Wafugaji  wa Ng’ombe wa maziwa (TDCU)  walio na hisa ya asilimia 42 wakati kampuni ya Uholanzi

(Dutch Oak) ina umiliki wa asilimia  48  kikiwa na uwezo wa kuzalisha lita 50,000 za maziwa ambapo upanuzi unaofanyika utakiwezesha kufikisha lita 120,000.

Mwenyekiti wa TDCU, Salim Rajab alimshukuru Rais  Magufuli kwa kutatua tatizo lililokuwa likiwakwamisha kwa muda mrefu na kuahidi kufanyia kazi maagizo yote yanayowahusu wafugaji.