In Summary

Tukio hilo lilitokea juzi wakati baraza hilo lilipokutana katika vikao vyake vilivyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Karimjee.


Dar es Salaam. Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam limemkosoa Meya wa jiji hilo, Isaya Mwita baada ya kubainika kutaka kuingiza agenda ambayo haikuwepo kikaoni.

Tukio hilo lilitokea juzi wakati baraza hilo lilipokutana katika vikao vyake vilivyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Karimjee.

Baada ya kuingia katika ukumbi huo, katibu wa kikao hicho, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana aliwaeleza kuwa ofisi yake ilipokea maombi kutoka Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart) waliokuwa wakitaka umiliki wa eneo la kituo cha mabasi ya Ubungo.

Baada ya Liana kuzungumza hayo, akafuata mwenyekiti wa kikao hicho, Mwita na kusema: “Nawaomba waheshimiwa madiwani mpokee kile alichokieleza katibu. Pia napenda kutambua uwepo wa wakilishi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

“Kutokana na hatua hii naomba niwape nafasi watu wa Tanroads watueleza walichokiandaa ili kujenga uelewa wa kile kinachokwenda kufanyika Ubungo kati ya Dart,” alisema Mwita ambaye ni diwani wa Vijibweni (Chadema).

Wakati wajumbe wa Tanroads wakijianda kutoa maelezo hayo ghafla wajumbe wa baraza hilo, Abdallah Chaurembo na Abdallah Mtolea walimwambia Mwita kwamba kilichotaka kufanywa na Tanroads hakipo kwenye ratiba.

“Mstahiki meya nakuomba urudi katika lengo la kikao hiki, ambalo ni uzinduzi wa gari la miili ya marehemu waliokosa ndugu na pia ufuate kanuni za uendeshaji wa kikao,” alisema Mtolea ambaye pia ni Mbunge wa Temeke.

Chaurembo ambaye pia ni Meya wa Temeke alishauri Tanroads wapewe muda wa kujipanga na kuwasilisha agenda yao siku nyingine.

Mwita alikubaliana na maombi ya wajumbe hao na kuahirisha kikao cha baraza hilo kisha kuitisha kikao cha kamati cha ndani.