In Summary

Lulu alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya kuua bila kukusudia


Dar es Salaam. Mama wa marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa amesema anatamani kwenda kumuona mwigizaji Lulu Michael anayetumikia kifungo cha miaka miwili jela lakini kwa bahati mbaya hawana maelewano na ndugu zake.

Akizungumza na MCL Digital leo Machi 14, 2018 Flora amesema yeye kama mzazi anaumizwa na hali anayopitia Lulu na anatamani kwenda kumuona ili kumpa moyo, ila ndugu wa mwigizaji huyo wanamuona kama ndiyo chanzo cha kufungwa.

Amesema wanaomlaumu wanapaswa waelewe kwamba yeye alishasamehe kwani hata angefungwa miaka 100, haiwezi kumfanya Kanumba arudi.

“Tangu Lulu kahukumiwa nimekuwa nikipokea lawama na watu kunitusi kuwa mimi ndiyo sababu, huku wakisahau kwamba mimi nilishasamehe kama binadamu na siyo niliyekuwa mlalamikaji katika kesi hiyo isipokuwa alishatakiwa na Serikali,” amesema Flora na kuongeza:

“Lakini yote namuachia Mungu kwa kuwa naamini kufungwa kwa msichana huyo hakuwezi kunirudishia mtoto wangu.”

Novemba 13, mwaka jana Lulu alihukumiwa kifungo cha miaka miwili baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia mwigizaji mwenzake, Kanumba.

Siku ya Kanumba

Wakati mwaka huu, Kanumba akiwa anafikisha miaka sita tangu afariki dunia ghafla, wasanii waliopitia mikononi mwake wanatarajia kuibeba siku ya Kanumba ambayo huadhimishwa Aprili 7 kila mwaka.

Akilizungumzia hilo, Flora amesema mwaka huu shughuli hiyo imebebwa na wasanii hao kupitia kikundi chao kinachoitwa Soweto.

Ameeleza ratiba ya siku hiyo, ni watu kukusanyika nyumbani kwake Kimara Temboni kuanzia asubuhi na baadaye wataelekea katika kaburi lake lililopo Kinondoni kwa ajili ya kufanya ibada, kisha kurejea tena nyumbani kwa ajili ya chakula cha pamoja.

Vilevile, siku hiyo kutazinduliwa jarida linaloelezea maisha ya Kanumba tangu kuzaliwa hadi kifo chake huku ndani yake kukiwa na filamu mbili zilizofanya vizuri ya ‘Uncle JJ’ na ‘This is It’.