Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imetangaza donge la Sh10 milioni kwa mtu atakayefanikisha kukamatwa kwa aliyekuwa mhasibu wake mkuu, Godfrey John Gugai anayetuhumiwa kujipatia mali nyingi kinyume cha Sheria ya Utumishi wa Umma.

Naibu mkurugenzi wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbung’o alisema jana kuwa Gugai hajulikani aliko, lakini “kama atakuja na kutoa ushirikiano ikiwamo kuthibitisha uhalali wa mali hizo, basi tutamwachia mali yake, lakini kwa nafasi yake kumiliki mali zote hizi zinatutia walakini.”

Septemba 14, 2016 Mwananchi lilikuwa gazeti la kwanza kuripoti habari za mhasibu huyo kufutwa kazi Takukuru baada ya kubainika kuwa ana utajiri wenye utata vikiwamo viwanja na majumba ya ghorofa.

Mei 16, taasisi hiyo ilijitokeza na kuanika utajiri unaokadiriwa kuwa wa thamani ya Sh3.5 bilioni unaodaiwa kumilikiwa na mhasibu huyo kinyume na sheria.

Miongoni mwa mali zilizotajwa ni viwanja 37, maghorofa saba, nyumba za kawaida tisa, magari matano na pikipiki.

Mali hizo kwa sasa zinashikiliwa na Takukuru kutokana na kibali ilichopewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mei 8, baada ya kupeleka maombi ya kuzikamata.

Mahakama hiyo ilitoa amri ya zuio la mali za Gugai anayetuhumiwa kujilimbikizia kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Ombi la zuio hilo lilitolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) chini ya kifungu namba 38(1)(a) na (b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007 katika shauri namba 13 la 2017.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mbung’o alisema: “Awali tulipomhoji alitoa ushirikiano, lakini tukiwa tunaendelea alitoweka na kwa taarifa tu amekuwa akitoka kwa magendo nje ya nchi. Kwa yeyote atakayefanikisha kumpata tutamzawadia Sh10 milioni.”

Alisema baada ya mhasibu huyo kutoweka walikwenda mahakamani na tayari kuna zuio la kufanya kitu chochote kwenye mali hizo ikiwamo kutouzwa wala kuendelezwa.

Naibu mkurugenzi huyo aliwaonya watumishi wa umma kutotumia vibaya madaraka waliyopewa kwa kuwa wakibainika Takukuru haitasita kuwachukulia hatua. Kutokana na maombi ya Takukuru mahakamani, mawakala na watu wengine wote wanaomwakilisha mhasibu huyo wamezuiwa kuuza au kuhamisha umiliki ama kuweka dhamana mali zote zilizowekewa zuio.

Pia, msajili wa hati aliagizwa kusajili zuio hilo kama kizuizi dhidi ya mali zote zilizotajwa, na msajili msaidizi wa magari alitakiwa kutoruhusu uhamishaji wa umiliki wa vyombo vya moto vilivyowekewa zuio mpaka mahakama itakapoelekeza vinginevyo.