In Summary

Wawekezaji waliopo katika maeneo hayo hawachangii elimu.

Dar es Salaam. Serikali imeshauriwa kuweka sheria madhubuti zitakazowabana wawekezaji na kampuni zinazofanya biashara kusaidia jamii inayowazunguka.

Ushauri huo umetolewa na wadau baada ya kuwasilishwa kwa ripoti iliyoelezea athari za mashamba ya kilimo cha biashara na migodi kwa haki za watoto kielimu.

Hoja hiyo imekuja baada ya ripoti kuonyesha kuwa licha ya kuwepo na wawekezaji katika maeneo mengi nchini wengi wao hawachangii kwenye elimu.

Akiwasilisha sehemu ya utafiti huo uliofanywa katika wilaya za Simanjiro na Urambo, mtafiti Lucy Kiowi amesema wawekezaji waliopo katika maeneo hayo hawachangii elimu.

Akitolea mfano wa Simanjiro amesema eneo hilo lina migodi mingi lakini kuna changamoto kubwa ya vyumba vya madarasa hali inayosababisha wanafunzi kurundikana darasani.

Kiowi amesema hali hiyo imeonekana pia Urambo ambapo kampuni zinazohusika na zao la tumbaku hazisaidii kuinua elimu katika wilaya hiyo.

"Yani watoto wanakimbia shule na kwenda kufanya kazi kwenye mashamba ya tumbaku. Wao wana mchango mkubwa kwenye zao hilo lakini hakuna wanachokipata na hata hakuna manufaa yoyote ambayo sekta ya elimu inapata,"

 

Hoja hiyo imeungwa mkono na watendaji akiwemo Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mirerani, William Wanga ambaye anasema licha ya wilaya hiyo kuwa na migodi mingi bado haina manufaa makubwa kwa wakazi.

 

Amesema kwa muda mrefu wilaya hiyo imekuwa na changamoto ya vyumba vya madarasa lakini mwaka huu kampuni moja ndiyo imejitolea kujenga madarasa matano na wamekalisha ujenzi wa jengo la mama na mtoto.

 

"Kiukweli wanachokipata ni kikubwa mno ikilinganishwa na wanachokirudisha kwenye jamii, wamekuwa wazito mno labda iwekwe sheria itakayowasukuma kufanya hivyo,"

 

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Uvinza, Benedict Katumba amesema "Uvinza kuna kiwanda cha kuvuna chumvi, watu wengi wanafanya kazi huko wakiwemo watoto lakini mwekezaji hajawahi kuchangia chochote kwenye jamii,"

 

"Huwa tunampelekea maombi na wakati mwingine kumshirikisha kwenye vikao, anaahidi atachangia lakini hajawahi kutekeleza ahadi yake," amesema Katumba.

 

Ripoti hiyo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 18 ya Mwalimu Julius Nyerere.