In Summary

Kufungwa kwa njia kuu ya magari ni sababu ya wafanyabiashara kutumia bodaboda kuvusha mahindi.

Tunduma. Biashara ya magendo ya mahindi mpakani Tunduma imesababisha kufurika kwa bidhaa hiyo sokoni hivyo bei kushuka kutoka Sh1,000 hadi Sh300 kwa kilo.

Taarifa zinasema baadhi ya wananchi raia wa Zambia wanatumia baiskeli na pikipiki kuingiza mahindi nchini kupitia njia za panya.

Mfanyabiashara mjini Tunduma, Jacob Haonga amesema wanapata mahindi mengi kutoka Zambia.

Haonga amesema kuingizwa kwa mahindi hayo kumeathiri biashara kwa kushuka bei. Amesema gunia la uzito wa kati ya kilo 90 na 100 linauzwa Sh36,000 badala ya Sh48,000 ilivyokuwa kati ya Juni na Julai.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mpande inayopakana na Nakonde nchini Zambia, Raphael Simkonda amesema biashara ya mahindi kutoka nchi hiyo imekithiri.

Amesema wakulima wamekuwa wakifikisha mahindi mpakani na kuwauzia wafanyabiashara wa Kitanzania ambao huyavusha kwa njia za magendo hadi kwenye masoko mjini Tunduma.

Amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mjini Tunduma huwatoza ushuru  lakini njia kuu ya magari imefungwa kwa amri ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, hivyo kuwafanya wafanyabiashara kutumia bodaboda kuvusha mahindi.

Kaimu Meneja wa Kituo cha Forodha Tunduma, Gerson Charles amesema awali, walikubali kuwatoza ushuru wa kuingiza mahindi nchini wakishirikiana na idara ya afya lakini baadaye walipokea agizo kutoka kamati ya ulinzi na usalama la kufunga njia iliyokuwa ikitumika.

Baada ya njia kufungwa, amesema walikamata magunia 2,300 ya mahindi yaliyokuwa yakiingizwa kwa siku moja.

Charles amesema idara iliamua kuwatoza ushuru wanaoingiza mahindi nchini ili kuwalinda wakulima wa ndani.

Mkuu wa Wilaya ya Momba, Jumaa Irando amesema biashara ya magendo ya mahindi ipo na imesababisha bei kushuka kutoka Sh1,000 hadi Sh300 kwa kilo moja.

“Hakuna ubaya kuingiza chakula katika masoko yetu, hali hiyo inasaidia kupunguza bei ya mazao katika masoko,’’ amesema Irando.

Hata hivyo, amesema ili kumlinda mkulima wa ndani Serikali imezuia baadhi ya njia zinazotumika kuvusha mahindi ya magendo.

Pia, amefanya mazungumzo na Bodi ya Mazao Mchanganyiko ili inunue mahindi wilayani Momba.