In Summary
  • Msajili wa Hazina, Dk Oswald Mashindano alibainisha jana Jumanne wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya, muda mfupi baada ya kuzindua tawi jipya la Benki ya Posta Tanzania (TPB) lililopo ndani ya soko la kimataifa la Mwanjelwa.

Serikali ipo mbioni kuzifanyia tathmini Benki za Kijamii ili kuona kama ni sahihi kuendelea nazo ama kufutiwa leseni baada ya kubainika zilizo nyingi hazifanyi vizuri kwa sababu baadhi zinaanzishwa kwa mashinikizo ya kisiasa.

Msajili wa Hazina, Dk Oswald Mashindano alibainisha jana Jumanne wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya, muda mfupi baada ya kuzindua tawi jipya la Benki ya Posta Tanzania (TPB) lililopo ndani ya soko la kimataifa la Mwanjelwa.

Alisema hadi sasa kuna benki za kijamii zaidi ya 10 baada ya benki moja kufutiwa leseni na sababu kubwa ya kutofanya vizuri ni kutokana na kuanzishwa huku zikiwa hazijakidhi vigezo muhimu jambo ambalo ni hatari kwa uchumi na wananchi wanaotumia benki husika.

“Ni niseme tu ukweli, hizi ‘community bank’ zilizo nyingi zilianzishwa kwa shinikizo la kisiasa kwa kulazimisha benki kuu kuruhusu kufunguliwa benki hata kama vigezo muhimu vya uanzishwaji wa taasisi hiyo havijatimia na ndio maana mwisho wa siku zinakufa jambo ambalo ni hatari kwa uchumi, na hivi sasa Serikali ipo mbioni kuzifanyia tathimini kama ni sahihi kuendelea nazo ama kuzipunguza,” alisema Dk. Mashindano.

Mkurugenzi Mkuu wa TPB, Sabasaba Moshingi alisema ni vigumu kupiga vita umasikini kama watu hususani wenye malengo ya kuanzisha na kufanya biashara kuogopa kuingia mkopo na taasisi za kibenki.

 

Alisema hakuna tajiri ama mfanyabiashara mkubwa aliyeweza kusimama mwenyewe bila ya kuingia benki kukopa fedha za kuendeshea biashara yake, hivyo aliwataka Watazania kuingia benki na kukopa bila kuogopa.

Alisema ‘Leo hii nchi ipo kwenye sera ya kuelekea uchumi wa viwanda, lakini hatutafanikiwa kwa muda mwafaka kama hatutathubutu kukopa fedha benki, na benki yetu tuwajali wateja kwa kuwapa mikopo ya masharti nafuu, kinachohitajika ni kuhakikisha mkopo wako unautumia kwa lengo kusudiwa na kurejesha kwa muda mwafaka’.

Mkazi wa Jijini Mbeya, Julius Mbembela alisema watu wengi wanatamani kukopa fedha kwenye taasisi za kibenki lakini kutokana na urasimu, mlolongo mrefu na masharti magumu yanawakatisha tamaa kukopa lakini mambo hayo yakiondolewa watu hawataogopa.

Mwisho.