Dar es Salaam. Licha ya Serikali na wadau mbalimbali kupigia kelele suala la ajira kwa watoto, wengi wameendelea kufanya kazi kwenye migodi na mashamba.

Utafiti uliofanywa na Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere umebaini kuwa watoto hufanya kazi katika maeneo hayo huku umaskini ukitajwa kuwa chanzo.

Utafiti huo ulifanyika katika migodi ya Mirerani, Buhemba na Uvinza na kwenye mashamba ya tumbaku (Urambo), mpunga (Mvomero) na nyanya (Ilula).

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, mtafiti Dk Novetha Kigombe alisema watoto wengi waliohojiwa wameeleza kuwa wanafanya kazi hizo ili wapate kipato kwa ajili ya familia zao.

Pia, alisema wazazi wamekuwa wakiwatuma ili washiriki kuongeza kipato cha familia kwa lengo la kukabiliana na umaskini.

“Katika kazi hizo watoto wanakutana na athari mbalimbali, kwanza wanaathirika kisaikolojia. Pia wengi wanaacha masomo ili wapate muda mwingi wa kufanya kazi,” alisema Dk Kigombe.

Katika kukabiliana na hali hiyo mwanasheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Joyce Komanya alisema ipo haja ya suala hilo kuwekewa sheria kali zaidi.

Alisema kama kungekuwapo na hatua kali za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya kampuni au mwekezaji anayeajiri watoto tatizo hilo lingepungua.

Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Profesa Penina Mlama alisema kufanyika kwa utafiti huo ni sehemu ya kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere.