In Summary

Samia amesema badala ya kukopa fedha na kufanyia mambo mengine, wanawake wahakikishe wanakuwa na vyoo bora.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ametaka vikundi vinavyotoa mikopo vifikirie kutoa ya ujenzi wa vyoo kwa wananchi wa hali ya chini na hasa vijijini.

Samia amesema hayo leo Alhamisi Desemba 7,2017 akizindua awamu ya pili ya kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira mjini Dodoma, iliyowakutanisha mawaziri, wakurugenzi na makatibu wakuu.

Amesema takwimu zilizopo ni kwamba, watu 892 milioni hawana vyoo kabisa duniani, huku takribani asilimia 70 ya wakazi wanaoishi kusini mwa jangwa la Sahara hawana vyoo bora.

“Lazima tujikite huko, wanawake badala ya kukopa fedha na kufanyia mambo mengine hakikisheni majumbani mwenu kuna vyoo bora,” amesema.

Samia amesema nchini asilimia 40.5 pekee ya kaya ndizo zenye vyoo bora, wakati takwimu zikionyesha kaya 600,000 hazina vyoo kabisa.

Amesema hali hiyo inabainisha kiini cha kuendelea kushamiri kwa maradhi ya kuambukiza na hasa kuhara na kipindupindu ambacho hadi sasa kinajitokeza katika baadhi ya mikoa na halmashauri.

Makamu wa Rais amesema vyoo vingi na hata vilivyo bora, havina sehemu za kunawia mikono. Amesema taasisi kadhaa zina upungufu wa huduma bora za vyoo.

Amesema madhara ya ukosefu wa miundombinu bora ya usafi wa mazingira
hayaishii katika kusababisha maradhi na vifo pekee bali inagusa sekta nyingine.

“Tanzania tunapoteza Sh440 bilioni kutokana na hali duni ya usafi hasa ukosefu wa huduma ya vyoo bora. Nchi yetu inaendelea kupambana na ugonjwa wa kipindupindu ambao hadi Novemba 12, 2017 watu 27,554 wameripotiwa kuugua na 432 walifariki,” amesema.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema awamu ya kwanza ya kampeni ya Taifa ya usafi wa mazingira ilianza mwaka 2012/2016 ikilenga ujenzi na matumizi ya vyoo bora, ikishirikisha halmashauri 163.

“Kupitia utekelezaji wa awamu ya kwanza, kaya 519,000 zilijenga vyoo bora, tulilenga kaya 600,000. Vituo vya afya 441 vimejengewa vyoo bora kutoka malengo ya vituo 250, hivyo tumefanikiwa upande huo kwa asilimia 146,” amesema Ummy.

Amesema lengo la wizara lilikuwa kuzifikia kaya 1 milioni, kutibu maji kwa kuweka dawa au kuyachemsha lakini wamezifikia kaya 934,437 ambazo zimeanza kutibu maji sawa na asilimia 93.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi,  Selemani Jafo amewaagiza wakurugenzi, wakuu wa wilaya na mikoa kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo awamu ya pili ya kampeni hiyo.