In Summary

Amesema amekubaliana na Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye ameondoka nchini leo alasiri Januari 14 baada ya kumaliza ziara yake ya siku moja, kuhakikisha wanahamasisha wafanyabiashara wa nchi hizo mbili kushirikiana  kujenga mazingira mazuri ya biashara.

Rais John Magufuli amesema kiwango cha mizigo inayokwenda Rwanda kupitia Bandari ya Dar es Salaam kimeongezeka mpaka kufikia tani 950,000 mwaka jana licha ya biashara katika ya mataifa hayo kupanda na kushuka.

Amesema amekubaliana na Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye ameondoka nchini leo alasiri Januari 14 baada ya kumaliza ziara yake ya siku moja, kuhakikisha wanahamasisha wafanyabiashara wa nchi hizo mbili kushirikiana  kujenga mazingira mazuri ya biashara.

Akizungumza na vyombo vya habari Ikulu jijini Dar es Salaam leo Januari 14, Rais Magufuli amesema biashara kati ya mataifa hayo mawili imekuwa ikipanda na kushuka na Serikali zote mbili zimepanga kupandisha biashara kwa kujenga mazingira wezeshi ikiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Isaka (Tanzania) mpaka Rwanda.

 

Amebainisha kwamba mwaka 2011, biashara kati ya Rwanda na Tanzania ilikuwa na thamani ya Sh106.5 bilioni, mwaka 2012 ilishuka mpaka Sh27.3 bilioni,  mwaka 2013 ilikuwa  Sh132.2 bilioni, mwaka 2014 Sh64.45 bilioni na mwaka 2015 ilikuwa Sh83.95 bilioni.

“Sasa unaweza ukaona trend, kwamba biashara imekuwa inapanda na kushuka. Sasa katika mzungumzo yetu tumekubaliana kwamba biashara kati ya nchi hizi mbili lazima ianze kupanda,” amesema na kuongeza,

 

“Na kupanda kwanza kunatokana na wananchi wa nchi hizi mbili wakubali kufanya biashara lakini jukumu jingine kubwa la Serikali ni kuhakikisha kwamba Serikali zote mbili inatengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara.”