In Summary

Dk Shika, ambaye jana aliachiwa kwa dhamana na polisi amesema haikuwa rahisi kujinasua kwa sababu alipata mateso makali na alijua ndiyo mwisho wa maisha yake, lakini kwa uhodari na nguvu za Mungu alifanikiwa kutoroka kutoka mikononi mwa watekaji hao.

Dar es Salaam. Dk Louis Shika ‘bilionea’ aliyejitokeza kununua majumba ya kifahari ya mfanyabiashara maarufu Said Lugumi ameelezea siku 28 za mateso aliyodai kuyapata baada ya kutekwa nyara nchini Urusi miaka 13 iliyopita.

Dk Shika, ambaye jana aliachiwa kwa dhamana na polisi amesema haikuwa rahisi kujinasua kwa sababu alipata mateso makali na alijua ndiyo mwisho wa maisha yake, lakini kwa uhodari na nguvu za Mungu alifanikiwa kutoroka kutoka mikononi mwa watekaji hao.

Hata hivyo aliendelea kusisitiza kuwa mpango wake wa kununua nyumba za Lugumi haujabadilika na kwamba ataishangaza dunia.

Alisema hayo jana jioni katika mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake Tabata Mawenzi baada ya kurejea kutoka mahabusu ya Kituo Kikuu cha Polisi alikoshikiliwa kwa siku sita akituhumiwa kuvuruga mnada huku leo akitakiwa kuripoti kituoni hapo saa tatu asubuhi.

Dk Shika, ambaye alidai kuwa alikwenda Urusi kwa masomo na baadaye kufanya kazi nchini humo alisimulia kuwa alitekwa na watu wasiojulikana Juni mwaka 2004 huku ‘watekaji’ wakimtaka awape Dola1.5 milioni za Marekani (Sh3 bilioni kwa sasa) ambazo hakuwa tayari kuzitoa licha ya kuwa na uwezo wa kuwapa.

“Nilipokamatwa walinipeleka sehemu huku nikipigwa, nikiteswa kwa siku 28 na nilijua ndio itakuwa kifo changu. Nilipigwa ngumi, niliteswa vikali, walitumia nyaya za umeme kunitesa, walinikata vidole kimoja kwa nyundo na viwili kwa panga, yote wakitaka niwape dola milioni moja na nusu,” alisema Dk Shika, ambaye mwandishi wa habari hizi alishuhudia kuona mkono wake wa kushoto ukiwa umekatwa vidole viwili na kidole kimoja mkono wa kulia.

“Sikuwa tayari kutoa, uwezo huo nilikuwa nao, siku 28 zilikuwa ngumu kwani chakula nilikula kile ambacho walibakiza wao, mwili wangu ulijaa damu, wale Warusi walinitesa sana kwani hata sikio langu (la kushoto, anamuonyesha mwandishi) limebondwabondwa, ni tofauti na hili la kulia hadi nafika Tanzania ni Mungu pekee anajua.”

Dk Shika alisema mateso hayo yalimsababishia maumivu makali ikiwamo kuvunjika mbavu tatu upande wa kulia na mbili kushoto ambazo bado hazijaunga vizuri.

Aliuhusisha mkakati wa kumteka na mmoja wa wafanyakazi katika kampuni yake aliyodai inaitwa Ralcefort ili kujipatia kiasi hicho cha fedha, lakini hawakufanikiwa baada ya kuwazidi ujanja na kutoroka.

Mwananchi lilipotaka kujua alitumia mbinu gani kutoroka ikiwa alikuwa hana nguvu na ndani ya jumba asiloweza kujua mlango ulipo, Dk Shika alidai, “ilikuwa siku moja wale watu walitoka na kumwacha mwenzao, akaanza kunywa pombe aina ya vodka na kujidunga unga, mimi nilipoona hivyo wakati huo nimefungiwa katika pipa la maji nilianza kufikiria mbinu za kumtoka.”

“Nilimhesabia tu muda, kuna muda ulifika nikamwona amelala na kwa kawaida mtu akilala ukimwangalia usoni anaweza kuamka, kwa hiyo mimi nikalibinua lile pipa na nikatoka, kule nje nilipotoka nilikutana na binti ambaye hakunisaidia.”

Dk Shika, ambaye huongea kwa kujiamini alisema baada ya kutoroka alipata msaada kutoka kwa wasamaria wema ambao walimchukua na kumpatia huduma ya kwanza wakati huo mwili wake ukiwa umeloa damu.

Alisema watu waliomsaidia walitaka awapeleke eneo alipotekwa, lakini siku ya kwanza hawakufanikiwa kwa sababu alikuwa hapajui vizuri ila siku ya pili walifanikiwa kupaona.

“Tulipofika mle ndani tulikuta damu imetapakaa chumba chote, kumbe wale watu walimuua yule mwenzao niliyemtoroka baada ya kudhani nilimpa fedha ili aniachie, wakadhani amewasaliti.

Kuhusu familia yake kumtenga kama alivyosema kaka yake anayeitwa Pelanya Lunyalula (84), katika mahojiano na Mwananchi, Dk Shika alisema, “mawasiliano mabaya, kama hatuwasiliani ni ukosefu wa mawasiliano, yawezekana mwenzangu akawa hana simu, sasa tutawasilianaje na sidhani kama nitakwenda (Simiyu) kwani kama wazazi wamekufa hata nikienda haitasaidia. Sasa ninachokiangalia ni kumaliza kwanza hili la kuzipata nyumba zangu.”

“Siku nikipeleka fedha nataka Yono (Kampuni ya Udalali iliyoendesha mnada huo) na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) waite waandishi wa habari waone na wautangazie umma,” alisema kwa kujiamini.

Polisi wamwachia kwa dhamana

Awali, kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alilieleza Mwananchi kuwa wamemwachia Dk Shika kwa kujidhamini mwenyewe baada ya kukosa mtu wa kumdhamini ila atakuwa akiripoti kila siku saa tatu asubuhi.

“Uchunguzi wa tuhuma dhidi yake unaendelea, lakini mpaka sasa hakuna mtu aliyefika kutaka kumuwekea dhamana, anaishi kama mtu wa nyikani. Nimeagiza watendaji wangu wamwachie kwa dhamana ajidhamini yeye mwenyewe na awe anakuja kuripoti kila siku,” alisema.

Njiani wakati akielekea kituo cha daladala cha Mnazi Mmoja baada ya kuachiwa na polisi, Dk Shika alikuwa kivutio kwa watu aliokuwa akipishana nao.

Hata allipopanda daladala la kwenda Tabata Mawenzi, kondakta alimkaribisha kwa kumweleza, “karibu mzee Shika”, huku ndani ya gari hilo watu wakipiga naye picha na alipowasili nyumbani kwake aligonga geti na kujitambulisha “choka mbaya bin mlalahoi” jambo lililowafurahisha waliojitokeza kumpokea.