In Summary
  • Siku hiyo ilipitishwa rasmi na na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Desemba 2011. Tangu wakati huo imekuwa ikiadhimishwa kila Oktoba 11. Hapa nchini Serikali na asasi mbalimbali hufanya matamasha ya kuelimisha wananchi namna ya kulinda haki za watoto wa kike, hasa umuhimu wa kupata elimu.

Jana Tanzania iliungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ambayo hapa nchini kitaifa ilifanyika wilayani Tarime Mkoa wa Mara. Siku hiyo ni mahususi katika kuhamasisha utatuaji wa changamoto zinazowakabili watoto wa kike, ikiwamo kulinda haki zao na kuwawezesha kufikia malengo yao.

Siku hiyo ilipitishwa rasmi na na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Desemba 2011. Tangu wakati huo imekuwa ikiadhimishwa kila Oktoba 11. Hapa nchini Serikali na asasi mbalimbali hufanya matamasha ya kuelimisha wananchi namna ya kulinda haki za watoto wa kike, hasa umuhimu wa kupata elimu.

Tunafahamu Tanzania yenye makabila zaidi ya 120, kila moja lina mila na desturi zake kuhusu malezi hasa kwa mtoto wa kike, lakini tangu tupate uhuru, bado mtoto huyo ameendelea kukabiliana na changamoto lukuki hasa vitendo vya ukatili.

Kuna baadhi ya maeneo ya Tanzania ambayo bado yanaamini mila za kukeketa, kitendo ambacho kimewafanya wale wasiopenda vitendo hivyo kuishi kwa wasiwasi na wengine kufikia hatua ya kutoroka nyumbani.

Vitendo vya ukeketaji vimekuwa chanzo cha tatizo la afya ya uzazi kwa mama na mtoto. Kwa mfano, mikoa ya Manyara, Mara, Dodoma, Arusha na Singida wasichana muda wowote wana wasiwasi wa kukeketwa kwa kuwa kitendo hicho kimekuwa sehemu ya utamaduni katika jamii nyingi za huko.

Siku hii pia inaadhimishwa wakati mtoto wa kike akiwa anakabiliwa na matatizo ya mimba na ndoa za utotoni. Wasichana wengi wanashindwa kumaliza elimu ya msingi ama kwa kupata ujauzito usiotarajiwa au kuolewa katika umri mdogo kutokana na shinikizo la wazazi.

Tunafahamu juhudi za Serikali ikiwamo kuweka sheria kali katika kumlinda mtoto wa kike, lakini utafiti unaonyesha kuwa takriban nusu ya wasichana wenye umri wa miaka 15 na 19 mkoani Katavi ni wazazi na robo yao walipata mimba za utotoni.

Kinachosikitisha ni kwamba watoto waliopewa mimba katika umri mdogo hukatisha masomo na ndoto zao huzima. Mabinti hawa wanakwenda mitaani kuongeza jamii ya kina mama wenye elimu ndogo na ambayo hupata wakati mgumu kujikwamua kiuchumi. Tunaamini ukandamizaji wa haki za wasichana kwa sehemu kubwa unaanzia kwenye familia. Kama jukumu la kumlinda na kumwendeleza mtoto wa kike, litaanzia kwenye familia, pengine changamoto hizo zingepungua.

Lakini, kinachoonekana pale mtoto wa kike anapopata tatizo la kufanyiwa ukatili wa aina yoyote, baadhi ya familia zimekuwa zikishirikiana na watuhumiwa kuficha uhalifu huo kwa ahadi ya fidia au aina nyingine ya malipo.

Kesi nyingi zimeshindwa kufunguliwa katika vyombo vya sheria au kuendelea kusikilizwa mahakamani, kwa kuwa upande mmoja umekataa kutoa ushirikiano.

Pamoja na kwamba elimu inaendelea kutolewa juu ya kumlinda mtoto wa kike, lazima ifahamike kuwa asasi za kiraia, polisi na Serikali kwa jumla hawatoweza kufahamu ukatili unaofanywa dhidi ya watoto awa kike kama familia au majirani wameshindwa kuripoti matukio hayo.

Tunawasihi wazazi, walezi, wanajamii wote na Serikali kuwajibika katika kulinda haki za mtoto wa kike kwa kuhakikisha anasoma vyema, analindwa dhidi ya mila kandamizi za ndoa za utotoni, ukeketaji na ukatili mwingine kama wa vipigo na kazi lukuki.

Waovu wote wafichuliwe na Serikali ichukue hatua kali dhidi ya wote wanaohusika ili kutengeneza Tanzania salama yenye fursa sawa za kimaendeleo kwa watoto wote.