In Summary
  • Mazungumzo ya kutafuta suluhu ndani ya SPLM yalianza mwaka 2015 jijini Arusha yakitanguliwa na mazungumzo ya awali yaliyoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu na aliyewahi kuwa makamu mwenyekiti wa CCM Bara, Mzee John Malecela na Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana .

CCM ni moja ya vyama vikongwe barani Afrika ambacho katika misukosuko ya ujio wa vyama vingi kimeweza kustahimili vishindo vya vyama vya upinzani na kuendelea kushika dola hatua iliyokifanya chama tawala nchini Sudan Kusini cha Sudan People’s Liberation Movement (SPLM) kutaka isaidie mgogoro wa ndani wa chama chao.

Mazungumzo ya kutafuta suluhu ndani ya SPLM yalianza mwaka 2015 jijini Arusha yakitanguliwa na mazungumzo ya awali yaliyoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu na aliyewahi kuwa makamu mwenyekiti wa CCM Bara, Mzee John Malecela na Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana .

Lengo ni kuhakikisha tofauti zilizojitokeza ndani ya chama cha SPLM kati ya Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake, Dk Riek Machar zinaondolewa kupitia mazungumzo na kuanza kujenga nchi yao ambayo ni changa zaidi barani Afrika na mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphrey Polepole anasema chama chake ni cha pili kwa mfumo na uthabiti wa kiitikadi barani Afrika baada ya chama tawala cha Afrika Kusini (ANC).

Kwa mantiki hiyo, baada ya kukubali maombi ya viongozi wa SPLM na kuanza mazungumzo ambayo baadaye yalitatizwa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 hapa nchini ni wakati muafaka kufufua mazungumzo hayo ambayo yanalenga kujenga amani na mshikamano wa kweli katika taifa hilo.

CCM ni ileile, sawasawa na kaulimbiu yake nikimaanisha wakati wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete aliyeanzisha mazungumzo na Rais wa sasa nguvu mpya ya Mwenyekiti wa chama, naibu makatibu wakuu, katibu wa itikadi na uenezi na katibu wa oganazaisheni ya mambo ya nje wanawajibu wa kufufua mazungumzo pale yalipoishia ili mwanachama mpya wa EAC aliyeonyesha imani kwenu ya kumaliza vita katika nchi yake inatimia.

Hapa ndipo ukongwe wa CCM unapotakiwa kuonekana kwa vitendo zaidi kwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho Rais John Magufuli kukumbushwa mahali mtangulizi wake alipoishia na kuendeleza mazungumzo kwa nia njema ya kuleta umoja na mshikamano wa kudumu katika taifa ambalo ni tajiri kwa mafuta barani Afrika.

Mgogoro wa kisiasa ambao umeiandama Sudan Kusini ulianza tangu Oktoba 2013 baada ya kuzuka mapigano katika mjini mkuu wake, Juba na kusambaa katika maeneo mengi ya nchi kwa kile kilichodaiwa kuwa Dk Machar alikuwa amepanga kufanya mapinduzi na kumwondoa madarakani Rais Kiir kupitia mkutano wa chama.

Licha ya mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro kupitia jumuiya ya kikanda ya nchi za pembe ya Afrika IGAD kufikia hatua ya kuweka saini makubaliano yaliyofanyika Addis Ababa, Ethiopia na Dk Machar kurejea Juba na kurejeshewa wadhifa wake wa Makamu wa Rais hali ya kutokuaminiana iliendelea na hatimaye alitoroka nchi na sasa anaaminika anaishi uhamishoni Afrika Kusini.

Kama walivyosema wenyewe kuwa mgogoro ulianzia ndani ya chama na kuwa usuluhishi uanzie ndani ya chama na kisha serikalini ni jambo jema ambalo linapaswa kuungwa mkono kwani pande zote zinafahamu chanzo na namna ya kuutatua kupitia mazungumzo ya kisiasa.

Ni wajibu wa CCM kuyafufua mazungumzo hayo tena ili kuendeleza diplomasia ya Tanzania kimataifa katika kufanikisha mazungumzo ya kutafuta amani kwa nchi jirani.

Mbali na CCM, ni imani yangu kuwa wadau wa maendeleo hasa Umoja wa Ulaya, Umoja wa Maendeleo ya Kikanda katika pembe ya Afrika (IGAD)Umoja wa Mataifa (UN), serikali za Norway, Marekani na Misri zitaendelea kusaidia mazungumzo hayo.

Filbert Rweyemamu ni Mwandishi wa gazeti la Mwananchi anapatikana kwenye namba 0754 94560 Arusha