In Summary
  • Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,149 kwa upande wa Tanzania, litapita katika mikoa minane na wilaya 24; wakati kwa upande wa Uganda litakuwa na urefu wa kilomita 296 kwenye wilaya nane.

Jana, Rais John Magufuli na mgeni wake, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni walizindua mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,149 kwa upande wa Tanzania, litapita katika mikoa minane na wilaya 24; wakati kwa upande wa Uganda litakuwa na urefu wa kilomita 296 kwenye wilaya nane.

Kwa hapa nchini bomba hilo litapita kwenye mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi iliyofanyika jana katika eneo la Chongoleani mkoani Tanga, Rais Magufuli alisisitiza umuhimu wa bomba hilo na akafafanua kwa kirefu jinsi ilivyokuwa vigumu kufikia uamuzi wa kulijenga kupitia Tanzania kuliko Kenya, kutokana na ushindani mkubwa uliokuwapo kati ya nchi hizo.

Ni imani yetu kuwa ushindani huo ulikuwa wa kibiashara tu na hauwezi kuwa sababu ya mahusiano yoyote mabaya miongoni mwa nchini wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli katika mazungumzo na Uganda, walikubaliana kwamba Tanzania itapata Dola12.5 za Marekani kwa kila pipa litakalosafirishwa kupitia bomba hilo ambalo kwa kuanzia litakuwa linasafirisha mapipa 216,000 kwa mwaka.

Vilevile, Uganda ambayo wataalamu wake walitumika kwa kiwango kikubwa kugundua mafuta hayo, itatoa wataalamu wake kufanya uchunguzi katika maziwa ya Tanganyika na Eyasi na endapo kutapatikana mafuta pia yatasafirishwa kupitia bomba hilo.

Kana kwamba haitoshi, Rais alimweleza Rais Museveni kuwa akitaka kupata gesi asilia kutoka Mtwara, Tanzania kwenda Uganda atapewa na itasafirishwa kupitia njia ileile na hivyo alimhakikishia ulinzi wa bomba hilo utakaohusisha askari 1,115.

Pamoja na kuwapo askari hao, sisi tunaamini kuwa suala la ulinzi wa bomba hilo linatakiwa kuwa la wananchi wote, wale wanaoishi karibu na eneo linakopita na wengine kwa ujumla kwa kuwa hili ni bomba la Watanzania wote na manufaa yake yatakuwa ya wote.

Ni kutokana na umuhimu huo, Watanzania wanatakiwa kulitazama kama fursa muhimu ya kiuchumi kwa manufaa ya mtu mmojammoja na ya taifa kuliko kuuchukuliwa kama mradi wa watu fulani wachache.

Vivyo hivyo, Watanzania wanatakiwa kujipanga kutumia fursa mbalimbali zitokanazo na mradi huo kwa sasa wakati wa ujenzi na hata baada ya mradi kukamilika.

Mathalan, mbali na ajira za Watanzania wakati wa ujenzi na ulinzi, wananchi wanatakiwa kujiandaa kuuza huduma mbalimbali kama za chakula, matunda, vinywaji, matibabu, usafirishaji na vifaa vya ujenzi kwa makandarasi na wafanyakazi wao.

Pia kampuni mbalimbali za ujenzi na uhandisi zinatakiwa kutazama mapema jinsi gani zitahusika na kunufaika na mradi huo mkubwa wa Dola 3.5 milioni za Marekani bilioni (Sh8 trilioni).

Na kamwe hatutarajii kuona vibweka vyovyote vya kuukwamisha mradi huo lakini kama kuna watu wanastahili fidia zozote kabla hawajapisha mradi huo walipwe bila vikwazo vyovyote.

Vilevile kama alivyodokeza jana kwamba picha zilikwishapigwa, nasi hatutarajii kuona watu ambao watataka kujenga nyumba au miradi mingine kwenye eneo la mradi huo ili kutega fidia.